(255) 0753559833

Historia ya TBBF

Kutokana na historia, mchezo wa wa kujenga mwili ulianzishwa kwa mara ya kwanza mnamo tarehe 24 Octoba 1995 katika ukumbi wa sinema wa Avalon, Dar es salaam wajenga mwili kumi na mbili walipanda jukwaani kuonesha misuli yao, lilikuwa ni onesho lenye mvuto wa aina yake na la kupendeza ambapo washiriki waliweza kuonesha mitindo mbalimbali ya utunishaji misuli kwa mpangilio wa kupendeza, lilikuwa ni onesho lilikonga nyoyo za watazamaji na hili ndio onesho lililoweka msingi wa mchezo wa kujenga mwili Tanzania

Mwanzilishi na mgunduzi wa mchezo wa kujenga misuli Tanzania si mwingine bali ni Fike Wilson. Bwana Fike Wilson ambae kwa sasa ni muigizaji na mwongozaji wa filamu pia ni mmoja kati ya watu watatu walioanzisha shirikisho la ujenzi wa mwili Tanzania (Tanzania Body Builder Federation T.B.B.F) . Bwana Fike alikuwa amevutiwa sana na kuhamasishwa na kanuni za ujenzi wa mwili za JOE WEIDER, akaanza kufanya mazoezi ya kujenga mwili mwenyewe halafu baadae kuanza kutoa mafunzo ya mbinu za kujenga mwili kwa watu wengine walienda kwake kujifunza mbinu za ujenzi wa kujenga mwili, katika GYM aliyokuwa anaimiliki, na ambayo baadae ikaja kuwa maarufu sana ikijulikana kwa jina la RED’S GYM, hiyo ilikuwa ni mwaka 1990 katika mji wa MBEYA, baada ya miaka mitano ya kuwasiliana na Joe Welder kwa njia ya barua kwa sababu ya kujifunza mbinu mbalimbali za ujenzi wa mwili, Fike Wilson akaamua kuhamisha GYM yake ya Red’s Gym Fitness Club na kuileta katika jiji la Dar es salaam, Sinza Kijiweni. Ilikuwa ni tarehe 18 June 1995 ambapo Fike Wilson alipokutana na wafanya mazoezi ambao walikuwa wakifanya mazoezi ya ujenzi wa mwili bila kufuata kanuni sahihi za ujenzi wa mwili huku wengi wao wakitumia vifaa duni vya ujenzi wa mwili

Mnamo tarehe 16 August 1995 Red’s Gym wakishirikiana na ofisi ya utamaduni ya Kinondoni walifanya semina ya ujenzi wa mwili kwa ajili ya wajenga mwili toka GYM mbalimbali jijini Dar es salaam na matokeo ya semina hiyo yalionekana katika onesho la kwanza la ujenzi wa mwili tarehe 18 Octoba 1995. Wajenga mwili wote waliohudhulia semina sasa walikuwa wanapanda jukwaanni kuonesha misuli mbele ya umati wa watazamaji, ndani ya ukumbi wa Avalon sinema. Mnamo tarehe 24 mwenzi wa nne mwaka 1996 katika ukumbi wa Sinema wa Star Light hoteli, washindani zaidi ya 26 toka maeneo yote ya Dar es salaam (Kinondoni, Ilala na Temeke) walipanda kushindana katika shindano la kwanza kabisa nchini Tanzania, shindano la Mr Dar es salaam 1996, washiriki ambao sasa wanashindana katika ukumbi wa Star light wengi wao ndio waliopata semina ya ujenzi wa mwili katika ofisi ya utamaduni na ndio sasa wanashindana. Washindani hawa zaidi ya ishirini ndio wao walioleta utukufu wa thamani ya mchezo wa kujenga mwili nchini Tanzania. Na mshindi wa kwanza kabisa katika historia ya mashindano ya kujenga mwili ya Dar es salaam 96 akawa ni Augustino Joseph na Fike Wilson akawa mshindi wa pili, Emily Adolf mshindi wa taji la urembo Tanzania 1995 alikuwa mgeni wa heshima na ndie yeye aliempatia, kumkabidhi taji la ushindi wa Mr. Dar es salaam mshindi wa shindano la Mr. Dar es salaam

Baada ya shindano la Mr. Dar es salaam kufanyika, umaarufu wa shindano ukasambaa Tanzania yote, mikoa kama ya Arusha, Mbeya, Morogoro, Tanga, Kilimanjaro, Dodoma na visiwa vya Zanzibar wakaamua kuanza kuandaa mashindano ya ujenzi wa mwili wakisaidiwa na muasisi wa mashindano ya kujenga mwili Bwana Fike Wilson

Mnamo tarehe 5 Desemba 1996 katika hoteli ya Kilimanjaro, kando ya bwawa la kuogelea shindano la kwanza la Mr. Tanzania lilifanyika na Fike Wilson akaibuka kidedea, Augustino Joseph akashika nafasi ya pili na Juma Selemani toka Zanzibar akashinda nafasi ya tatu, shindano lilidhaminiwa na TASOTA (Tanzania Society of Travel Agents) MULT-LOCK na SALAMA CONDOM na mgeni wa heshima alikuwa barozi mheshimiwa mama/bibi Marry Yvonne Pool na shindano lilisimamiwa na msimamizi ambae alikuwa katibu mkuu wa baraza la michezo la Taifa Marehemu Samson Kayobyo

Mpaka hapo mchezo wa kujenga mwili ukaanza kupata umaarufu kwa kasi ya juu, huku vyombo mbalimbali vya habari vikiupa kipaumbele katika kuandika katika makala zao maalum

Baada ya mafanikio ya shindano la Mr. Dar es salaam na Mr Tanzania bwana Fike Wilson akaona na kufikiri kuanza kuanzisha shirikisho la kujenga mwili Tanzania ili mchezo wa kujenga mwili Tanzania ili mchezo wa kujenga mwili upate kustawi kwa mapana na marefu akiungana na washirika wake wenye mawazo yenye ustawi kama wake, akiwemo bwana Francis Mapugilo( Katibu Mkuu wa sasa) na bwana Nemes Chilawala (Mwenyekiti wa sasa) wakaungana pamoja na kuanzisha shirikisho la ujenzi wa mwili Tanzania (T.B.B.F)

Shindano la kujenga mwili la Mr Tanzania limekutana na misukosuko mingi ya hapa na pale. Shindano la pili la Mr Dar es salaam lilikaribia kusimamishwa muda mchache kabla ya kuanza huku umati mkubwa wa mashabiki wa shindano wakiwa nje ya ukumbi wa FM club wakati ule wakiwa wanakata tiketi za kuingia ukumbini, shindanno lilisimamishwa na jeshi la polisi kwa amri toka kwa Afisa utamaduni wa mkoa wa Dar es salaam wakati ule bwana Salimi Dossi. Shindano lilisimamishwa na polisi. Na mashabiki ilibidi warudi nyumbani wakiwa shingo upande, afisa utamaduni Salim Dossi alikuwa analalamika anasema mchezo wa ujenzi wa mwili si mchezo bali ni “ mchezo wa kutafuta wanaume wazuri” kwa hiyo basi kutokana na huu mchezo kuchezwa wanaume wakiwa wamevaa vichupi vya kupandia jukwaani mbele ya waandishi na vyombo vya habari. Ni mchezo ambao haufahi kabisa kwa jamii ya watanzania. Mchezo kama haufai unaharibu fikra za watu wanaoutazama kwa hiyo ni lazima upigwe marufuku. Hapa itakuwa ni jambo zuri kuweka jina la katibu tawala wa mkoa wa wakati ule mama SALOME SIJAONA katika historia ya mchezo huu wa kujenga mwili ambapo baada ya kumtembelea ofisini akaja kujua kwamba kweli sisi ni wanamichezo akaomba kama tunatambulika na baraza la michezo la Taifa baada ya kumuonesha nyaraka zote za kiserikali akatutambua na akaandika barua kutaka ufafanuzi zaidi kuhusu mchezo wa kujenga mwili. Ndipo Salim Dossi akasema amri ya kusimamishwa wizarani na hiyo sio kwa ujenzi wa mwili tu bali hata mambo ya mashindano ya urembo pia hayatakiwi hii ni amri toka wizara ya utamaduni, kazi, vijana na michezo, baada ya ushauri wa bwana Elikunda Matemu ambae alikuwa mkurugenzi wa utamaduni. Elikunda Materu alisema “ujenzi wa mwili na mashindano ya urembo si sehemu ya utamaduni wetu na kutembea uchi ni mwiko hapa Tanzania”

Maandamano makubwa yakafinya katika mitaa ya jiji la Dar es salaam kupinga hii sheria na mwisho wake mamlaka ikaamua kuketi na kujadili hili jambo na matokeo yakaanikwa kuwa washiriki wa shindano la urembo na shindano kujenga mwili la Mr. Tanzania hawatakiwi kuvaa mavazi ya nusu uchi na makubaliano yakafikiwa na kwa makubaliano hayo mashindano yakaruhusiwa kuendelea. Mr. Dar es salaam mwaka 1997 yakarudi tena jukwaani sehemu ile ile F.M CLUB KINONDONI na GUINESS BREWING LIMITED walikuwa ni wadhamini wa onesho, SOLOMON NASUMA akawa mshindi wa Mr Dar es salaam 1997 na JIMMY BOMBAY akawa mshindi wa pili na marehemu ROBINSON WILSON (ROBY) akawa mshindi wa tatu

Mnamo tarehe 18 Desemba 1997 shindano la pili la Mr. Tanzania lilisimamiwa na bwana FRANCIS ANDONI MAPUGILO likafanyika chini ya udhamini wa Guiness Brewing Limited, Fike Wilson akaibuka kidedea na kushinda taji la Mr Tanzania kwa mara ya pili akiwashinda washiriki wengine ishirini na mbili toka mikoa kumi na moja ambayo ni Mbeya, Tanga, Arusha, Kilimanjaro, Rukwa, Pwani, Morogoro, Dodoma, Shinyanga na Dar es salaam. George Adolph toka Tanga akawa mshindi wa pili na Augustino Joseph akawa mshindi wa tatu. Muheshimiwa waziri wa michezo na utamaduni Bwana WILLIAM LUKUVI alikuwa ndie mgeni wa rasmi

Mnamo tarehe 19 mwezi wa nne mwaka 1998 mashindano ya tatu ya wajenga mwili yalifanyika chini ya udhamini wa Guiness Brewing World Wide Limited kwa mara nyingine tena. Sasa hivi shindano la Mr Dar es salaam 1998 likawa linaitwa Mr Guiness 1998. Mr Guiness Dar es salaam 1998 likafanyika na Solomon Nasuma akashinda taji tena, Kassim Mpaila alikuwa ni mshindi wa pili na Dulla Mohamed akawa wa tatu. Baada ya shindano la Mr. Guiness Dar es salaam 1998 kikanda kuanza. Kulikuwa na ushindani katika kanda tatu, UKANDA WA MASHARIKI, UKANDA WA KUSINI na UKANDA WA MAZIWA MAKUU, washndi wa kanda zote tatu na washindi wao wa pili na watatu wakaja kushindana kwenye shindano la tatu la Mr. Tanzania 1998. Kambi ya washiriki iliwekwa kwenye kituo cha YMCA katikati ya jiji. Shindano la Mr Guiness Tanzania lilifanyika kwenye ukumbi wa Silent Inn Club Mwenge. Mheshimiwa naibu waziri wa elimu, michezo na utamaduni bwana Bujiku Sakila alikuwa ndie mgeni rasmi, George Adolph akaibuka kidedea, Solomon Nasuma akawa mshindi wa pili na Mohamed Ali akawa mshindi wa tatu. Washindi sita waliofika fainali wakaunda timu ya Taifa ambao wakapata mualiko wa kushiriki kwenye shindano la Mr. Afrika ujenzi wa mwili katika jiji la Cairo Misri mnamo tarehe 20 mwezi wa pili mwaka 1999. Safari ya kueleke Misri ilidhamiminiwa na Tanzania Breweries Limited (TBL) George Adolph akashinda medali ya shaba

Mashindano ya Mr Tanzania ya mwaka 1999 yalifanyika kwenye hoteli ya Capa Cabana Masaki ambao ndio walikuwa wadhamini wa onesho. Mshindi wa shindano alikuwa ni Solomon Nasuma, mshindi wa pili alikuwa ni Ndeyanka Omari na wa tatu alikuwa Dulla Saidi. Mwaka 2000 mshindi wa Mr. Tanzania alikuwa ni Nyakashi Ntwenya, mshindi wa pili alikuwa James Sunga na wa tatu alikuwa marehemu Julius Mapambano, shindano lilifanyika kwenye hoteli ya White Sand, wadhamini pekee walikuwa ni Tusker Milk Stout. Shindano la Mr Dar es salaam lilifanyika Mambo Club Oysterbay ambayo sasa inatambulika kama Maisha Club. Ally Ramadhani “Van Damme” akaibuka mshindi, Dulla Saidi akawa mshindi wa pili na Juma Hassan akawa mshindi wa tatu

Mwaka 2001 na 2002 hakukuwepo na mashindano kutokana na ukosekanaji wa wadhamini

Mwaka shirikisho la ujenzi wa mwili la Dar es salaam ambalo ni mshirika mdogo wa TBBF kwa kushirikiana na DESTINATIN TRAVEL AGENCY LIMITED ambao walikuja kuwa kama wadhamini kwenye bodi ya mashindano ya Mr Dar es salaam. Shindano lilifanyika tarehe 22 Mwezi may 2003 ukumbi wa F.M CLUB KINONDONI na bwana Rodgers Hamis akaibuka mshindi, James Sunga akwa mshindi wa pili na Kurwa Omari akawa mshindi wa tatu

Kuanzia mwaka 2004 mpaka 2005 kwa bahati mbaya tena kutokana na ukesefu wa wadhamini shindano halikufanyika. Mnamo mwaka 2006 mchezo ukarudi tena na safari hii kwa kuwaalika ngazi zote za wajenga mwili kuanzia kanda zote tatu za Ilala, Kinondoni na Temeke REDS GYM na KILIMANJARO FITNESS walikuwa ndio wadhamini wa shindano. Shindano likafanyika kwenye hoteli ya 92 Sinza shekilango road tarehe 14 mwezi wa nane 2006 wakati kundi la wajenga mwili 22 walipoingia kwenye onesho na Kurwa Omari akaibuka mshindi wa MR Dar es salaam kwa kuwashinda washiriki wengine 21, Frank Lupangile akawa mshindi wa pili na marehemu Omari Fundikira akawa mshindi wa tatu

Mwaka 2007 Mr Dar es salaam ikafanyika tena kwa kutumia jina la mdamini kama Mr Mobipawa 2007 likafanyika chini ya udhamini wa MOBIPAWA SIMU NI PESA. Mashindano ya kujenga mwili ya MR MOBIPAWA yalifanyika kwenye fukwe za Coco Oysterbay tarehe 12 Desemba 2007, washindani 20 waliingia kwenye mtanange, Bedui Omari akaibuka mshindi wa Mr Mobipawa 2007 na Vistus Mwami akawa mshindi wa pili na Robert Samson akawa mshindi wa tatu

Baada ya 2007 zikaja siku za giza za huu mchezo na mashindano kutokana na kukosekana kwa wadhamini kwa sababu kwa wakati hhuo dunia ilipata mtikisiko kiuchumi kutokana na kushuka kwa thamani ya dola ya marekani. TBBF na wadau wake toka siku hiyo wakaanza kutoa semina kuhusu ujenzi wa mwili kwenye baadhi ya gym nchini, Nyakashi Ntwenga Mr. Tanzania wa sasa na kamati ya mashindano ya T.B.B.F chini ya uongozi wa bwana Fike Wilson, Nemes Chilawala na katibu mkuu Francis Andon wanafanya kila jitihada kuhakikisha huu mchezo unapata mafanikio

Kwa sasa tunaweza kuona kuwa watanzania wengi wanaonekana kujali afya zao na tamaduni ya gym imefumka. Club kubwa za mazoezi zimeanza kutoa ushauri wa kuimarisha afya. Wajenga mwili sasa wamekuwa wakufunzi na washauri wa mambo ya afya kimazoezi. Wavula na wasichana wameanza kwenda gym ili wawe imara na warembo kutokana na hamasa yao juu ya ulimbwende na kuigiza. Wakati ukifanya mazoezi kwa kuhamasika na malengo yako unaanza kujihisi vizuri na kuwa imara zaidi na unahitaji changamoto.

T.B.B.F iliamua kuwapa hawa wavulana jukwaa la changamoto na kushindana kwenye kundi la Mr. Tanzania handsome na Mr. Tanzania Photogenic pamoja na taji la Mr. Tanzania mnamo mwaka 2017 ambalo lilianza tena kwa shauku kubwa na nguvu zaidi kutoka Pilipili Entertainment Company Limited ambao ni wandaaji maarufu wa matukio na watengenezaji wa maonesho yenye ubora zaidi.